Luke 5

Kuitwa Kwa Wanafunzi Wa Kwanza

(Mathayo 4:18-22; Marko 1:16-20)

1 aSiku moja Isa alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti,
Yaani Bahari ya Galilaya.
watu wengi wakiwa wanasongana kumzunguka ili wapate kusikia neno la Mungu,
2akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao. 3 cAkaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.

4 dAlipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”

5 eSimoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”

6 fNao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika. 7Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.

8 gSimoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni mwa Isa na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!” 9Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata. 10 hVivyo hivyo wenzake Simoni, yaani Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walishangazwa pia.

Ndipo Isa akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.”
11 iHivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata.

Isa Amtakasa Mtu Mwenye Ukoma

(Mathayo 8:1-4; Marko 1:40-45)

12 jIkawa siku moja Isa alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Isa, alianguka chini mpaka uso wake ukagusa ardhi, akamsihi akisema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.”

13Isa akanyoosha mkono wake, akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Na mara ukoma wake ukatakasika.

14 kIsa akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu yeyote, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”

15 lLakini habari zake Isa zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wowote. Makutano makubwa ya watu yalikuwa yakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16 mLakini mara kwa mara Isa alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.

Isa Amponya Mtu Mwenye Kupooza

(Mathayo 9:1-8; Marko 2:1-12)

17 nSiku moja Isa alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa. 18 oWakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Isa. 19Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya matofali, wakamteremsha yule mgonjwa kwa mkeka wake hadi katikati ya ule umati pale mbele ya Isa.

20 pIsa alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”

21 qMafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

22Isa akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 23Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 24 rLakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 25Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake, akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu. 26 sKila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”

Isa Amwita Lawi

(Mathayo 9:9-13; Marko 2:13-17)

27 tBaada ya haya, Isa alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.” 28 uNaye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.

29 vKisha Lawi akamfanyia Isa karamu kubwa nyumbani kwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao. 30 wLakini Mafarisayo na walimu wa sheria waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Isa, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

31Isa akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. 32 xSikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”

Isa Aulizwa Kuhusu Kufunga

(Mathayo 9:14-17; Marko 2:18-22)

33 yWakamwambia Isa, “Wanafunzi wa Yahya na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”

34 zIsa akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati yuko pamoja nao? 35 aaLakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.”

36 abIsa akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kutoka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, atakuwa amechana nguo mpya, na kile kiraka hakitalingana na ile nguo iliyochakaa. 37 acHakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo yote itamwagika. 38 adDivai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya. 39 aeWala hakuna mtu anayependelea divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani, bali husema, ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’ ”
Copyright information for SwhKC